Na Lucy Lyatuu
INAKADIRIWA kuwa zaidi ya asilimia 34 ya vifo nchini Tanzania vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza.
Magonjwa hayo ni yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa kama tatizo la moyo na mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kisukari,magonjwa ya akili,sikoseli na mengineyo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Roida Andusamile wiki ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) huadhimishwa wiki ya pili ya Oktoba kila mwaka.
Amesema kwa mwaka 2025 maadhimisho haya yanaadhimishwa kuanzia leo Oktoba 10 hadi 15 kwa lengo la kuongeza uelewa wa umma kuhusu madhara ya magonjwa yasiyoambukiza,umuhimu wa kuchukua hatua za Pamoja katika kuyazuia na kuyadhibiti.

Kauli mbiu ya mwaka 2025 ni chukua hatua dhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambayo inasisitiza wajibu wa kila mmoja katika kuchukua hatua za kulinda afya yake na kusaidia jamii kuwa na Maisha yenye ustawi.
Roida amesema magonjwa yasiyoambukiza ni Pamoja na saratani, kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, afya ya akili, figo, selimundu na baadhi ya magonjwa ya njia ya hewa.
Amesema takwimu za kidunia na za hapa nchini zinaonesha idadi ya wagonjwa kuongezeka,inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 34 ya vifo nchini Tanzania vinatokana na magonjwa hayo.
“Kwa kuwa dalili za magonjwa hayo huchelewa kutambulika na yanaweza kuzuilika, wizara ya afya inawahimiza wananchi kufanya uchunguzi mara k wa mara ili kugundua magonjwa mapema na kuanza matibabu, kuzingatia mtindo bora wa Maisha kwa kula mlo sahihi yenye virutubisho, kufanya mazoezi angalau daika 30 kila siku, kuacha matumizi ya tumbaku na pombe na matibabu ya mapema ili kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza,” amesema.

