Na Mwandishi Wetu
TANGA: WANANCHI wametakiwa kuwa waangalifu na wenye uelewa wa kutosha wanapochukua mikopo ili kuepuka kuingia kwenye mzigo wa madeni usio na tija, hususan mikopo yenye riba kubwa inayodaiwa kuwanyonya wananchi.
Wito huo umetolewa na Meneja Masoko na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF, Linda Mshana, leo Januari 20, 2026, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Maadhimisho hayo yalianza Januari 19 na yanatarajiwa kumalizika Januari 26, 2026.
Mshana amesema mfuko wa SELF unaendelea kutoa elimu sahihi ya fedha kwa wananchi, ikiwemo matumizi bora ya mikopo, mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo pamoja na maswali muhimu ya kuuliza wanapohusiana na taasisi za kifedha,
Hatua itakayowasaidia kuepuka changamoto za mikopo isiyo rafiki.
Ameongeza kuwa wananchi wa mkoa wa Tanga wanakaribishwa kufika katika maadhimisho hayo ili kupata elimu ya fedha, kufahamu fursa zilizopo pamoja na kujifunza njia mbalimbali za kujiendeleza kiuchumi.
Kwa mujibu wa Mshana, SELF ina mikopo ya aina mbalimbali inayolenga makundi tofauti yakiwemo wafanyabiashara wa nafaka, wafugaji, wavuvi na wakulima.
Aidha, mfuko huo pia hutoa mikopo ya kuboresha makazi kwa wananchi wanaotaka kuboresha nyumba zao ili zipate muonekano bora zaidi.
“Kwa wale wanaotaka kuanzisha au ambao tayari wanaendesha taasisi za kifedha zinazotoa mikopo na wamepata kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), SELF inatoa fursa ya kuongeza mtaji kupitia mikopo,” amesema.
Amebainisha kuwa suala la riba limekuwa likiulizwa mara kwa mara, hali inayoonesha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu kuhusu namna sahihi ya kukokotoa riba na kuelewa gharama halisi za mikopo.
Mshana ameongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kupitia mfuko wa SELF kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa mpana wa masuala ya kifedha.
Amesema mfuko wa SELF ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha, inayojikita katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo yenye masharti nafuu, sambamba na kutoa elimu ya fedha na bima.

