Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameridhishwa na utekelezaji wa miradi 81 ya dharura iliyosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), akieleza kuwa imekamilika kwa wakati na kwa viwango vya juu vya ubora.
Akifungua Mkutano wa 21 wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS mkoani Morogoro, Ulega amesema mafanikio hayo yanadhihirisha kukua kwa uwezo wa makandarasi wazawa na wataalamu wa ndani.
Amefafanua kuwa miradi hiyo, iliyohusisha ujenzi wa madaraja na makalvati kupitia mpango wa CERC, imekuwa msaada mkubwa katika kupunguza athari za mvua na mafuriko.
Ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha, akisema uwekezaji huo umeanza kuleta matokeo chanya, ikiwemo kupungua kwa uharibifu wa miundombinu licha ya mvua zinazoendelea kunyesha mwaka huu.
Ulega amesisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya maeneo yenye uhitaji wa madaraja ya kisasa, huku akiwataka watumishi wa TANROADS kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu.
Pia ameelekeza matengenezo ya barabara na madaraja yafanyike kwa wakati ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Aidha, amesisitiza utekelezaji wa mpango wa kupendezesha barabara kwa kupanda miti ya kivuli na matunda pamoja na kuimarisha taa za barabarani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za awali kwa ujenzi wa barabara ya Bigwa–Kisaki, akibainisha kuwa wananchi watanufaika na mradi huo.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta, amesema mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi, huku Menejimenti ikiahidi kuendelea kutekeleza maelekezo yote kwa ufanisi.

