Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewashauri vijana kujiunga na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) kupata ujuzi na maarifa vitakavyo wawezesha kukuza uchumi wao na Taifa.
Pinda ametoa ushauri huo kwenye Maadhimisho ya miaka 30 ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema ufundi stadi na ubunifu vinavyaotolewa na VETA ni muhimu katika maisha ya kila siku, hakuna anayeweza kukwepa, kwani ni sehemu ya maendeleo ya Taifa.

Amewashauri vijana kutumia fursa hiyo adhimu, kupata maarifa ya ufundi stadi, kupitia vyuo vya VETA, ikiwemo vingine vya watu binafsi ambavyo vinaaminiwa na Mamlaka hiyo kwa kujiunga kwani vitakawajengea fursa baadaye.
“Naamini hata Mkurugenzi wa atachochea zaidi katika mafunzo haya muhimu ya vijana, kuwavutia zaidi kujiunga, kusonga mbele zaidi kimaendeleo, kupitia ujuzi huu muhimu wa vyuo hivi” amesema.

“Katika matumizi ya kawaida ya nyumbani kuna umeme na maji, vyote hivi vikiharibika, lazima umuite fundi atengeneze huwezi kufanya mwenyewe, hii inaonyesha umuhimu wa wataalamu hawa wanaoandaliwa na Veta,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore ameshukuru Pinda kwa kufika kwenye maadhimisho hayo, kwa kuwa anashuhudia matunda ya mchango wake mkubwa alioutoa kwa Mamlaka hiyo kupitia uboreshaji wa sera na ushauri wake wa mara kwa mara anaowapa.
Kadhalika amewapongeza washiriki wa maadhimisho hayo ya miaka 30, huku akiwataka wananchi kuendelea kujiunga na VETA kwani, mtu yeyoye anaruhusiwa kujiunga na mafunzo hayo.