Waziri Mkuu wa Namibia, Dkt. Tjitunga Elijah Ngurare (wa nne kutoka kushoto), akiwa na viongozi na washirika wa SGCI baada ya ufunguzi wa jukwaa la washirika mjini Windhoek. Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, ni wa tatu kutoka kushoto.
Na Mwandishi Wetu
WINDHOEK, NAMIBIA: WAZIRI Mkuu wa Namibia, Dkt. Tjitunga Ngurare, ameonya kuwa kushindwa kwa Afrika kuwapa vijana fursa za elimu, utafiti, ubunifu na ajira kunaweza kuigharimu bara hilo, akisema vijana ni rasilimali kubwa zaidi ya Afrika.
Dkt. Ngurare ametoa kauli hiyo Septemba 30, 2026, alipofungua Jukwaa la Washirika wa Mpango wa Kuimarisha Taasisi za Ufadhili wa Utafiti Afrika (SGCI) mjini Windhoek, Namibia.
Amesema serikali na taasisi za utafiti zinapaswa kuwaandaa vijana kutumia vipaji na mawazo yao katika kutatua changamoto za jamii, badala ya kuwaacha bila fursa za kuyaendeleza.
“Ikiwa hatuwasikilizi vijana wetu, hilo ni bomu linalosubiri kulipuka,” amesema.
Amesema Afrika inahitaji kuwekeza zaidi katika elimu, utafiti na ubunifu ili kuwapa vijana uwezo wa kutengeneza ajira badala ya kusubiri ajira zilizopo.
Dkt. Ngurare ameeleza kuwa akiwa mwanafunzi alishiriki mashindano ya sayansi yaliyomsaidia kuona fursa ya kuendelea na masomo ya sayansi. Katika mashindano hayo, alichunguza namna mmea unaopatikana katika Jangwa la Namib unavyoweza kustahimili mazingira magumu.
Kwa mujibu wake, uzoefu huo unaonyesha umuhimu wa kuwafikia wanafunzi mapema, kuwapa nafasi ya kujaribu mawazo yao na kuwaunganisha na taasisi zinazoweza kukuza vipaji na ujuzi wao.
Amesema uwekezaji kwa vijana haupaswi kuishia darasani, bali unapaswa kuhusisha utafiti unaoweza kuzaa bidhaa na huduma, kuboresha maisha ya wananchi na kufungua fursa za kiuchumi.
Aidha, amehoji ni lini Afrika itaanza kuzalisha kampuni zake kubwa za teknolojia na kutumia kikamilifu uwezo wa wataalamu wake katika kujenga uchumi wa bara hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesema taasisi za ufadhili wa utafiti zina wajibu wa kuhakikisha tafiti zinazofadhiliwa zinajibu mahitaji halisi ya jamii.
Dkt. Nungu, aliyetoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa jukwaa hilo, amesema COSTECH itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi hizo ili maarifa ya kisayansi yageuzwe kuwa sera bora, suluhisho zinazotumika na kuboresha maisha ya wananchi.
Nchini Tanzania, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela vina viti vya utafiti chini ya Mpango wa O.R. Tambo Afrika, unaosaidia kujenga timu za utafiti na kuwanoa wanasayansi vijana katika maeneo ya afya na teknolojia.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!