Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 14

ESAP Yaleta Teknolojia Kupunguza Gharama Za Wachimbaji Wadogo

Na Lucy Ngowi

GEITA: KAMPUNI ya ESAP Mining Services Ltd inaandaa kuleta mashine ndogo za uchimbaji wa chini ya ardhi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za shughuli zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Yahya Puyaga amesema hatua hiyo inafanyika kupitia mazungumzo na kampuni mbalimbali za nje kwa ajili ya ubia wa kiteknolojia na kuleta vifaa vinavyoendana na mahitaji halisi ya wachimbaji wadogo.

Habari Picha 13939

Amesema kampuni imebaini kuwa sehemu kubwa ya wachimbaji wadogo hutumia mfumo wa uchimbaji wa chini ya ardhi, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mashine ndogo zinazoweza kufanya kazi katika mazingira hayo.

“Mtambo uliopo unafaa zaidi kwa uchimbaji unaofanyika kutoka juu, wakati wachimbaji wadogo wengi wanatumia mfumo wa uchimbaji wa chini ya ardhi,” amesema.

Kwa mujibu wa Puyaga, kampuni hiyo pia inatarajia kuzalisha bidhaa maalum kwa wachimbaji wadogo kupitia kiwanda chake kilichopo Bukombe, Geita, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa baadhi ya vifaa vya uchimbaji ndani ya nchi.

Amesema bidhaa inayozalishwa katika kiwanda hicho tayari inatumika katika shughuli za uchimbaji wa chini ya ardhi, huku gharama yake ikiwa na ushindani ikilinganishwa na bidhaa zinazotumika kwa sasa.

Habari Picha 13940

Puyaga amesema ESP inaendelea kushirikiana na wazalishaji wa nje ili kupata teknolojia na vifaa zaidi vitakavyokidhi mahitaji ya wachimbaji wadogo na kuboresha ufanisi katika shughuli zao.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.