Na Danson Kaijage
DODOMA: WATANZANIA wametakiwa wawe makini kwa kutowachagua watu wanaosaka uongozi kwa kutumia nguvu ya rushwa.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (EAGT) Gosheni, Evance Mushi ametoa angalizo hilo alipokuwa akihubiri na kueleza jinsi ya kuwapata viongozi bora.
Mushi amesema wagombea wenye sifa wanatakiwa kugombea nafasi mbalimbali na kunadi sera zao ila wajiepushe na yale yanayoweza kuwa machafuko mbele za Mungu.
Amewataka wagombea kutojihusisha na vitendo vya kuwashawishi wapigakura kwa kutoa rushwa au kwenda kwa waganga wa kienyeji.

Pia amewakemea wale ambao wanatafuta nafasi mbalimbali kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji na kueleza kuwa taifa haliwezi kuendeshwa na watu wa aina hiyo bali wacha Mungu wenye hofu ya Kimungu.
“Ni aibu kuwa na taifa linaloongozwa na viongozi wanaoingia madarakani kwa njia ya rushwa au kwa nguvu za giza viongozi wa aina hiyo ni wazi kuwa watakuwa mafisadi na wasiokuwa na uchungu wa rasilimali za Taifa na badala yake watakuwa watu wa kutafuta faida yao binafsi,” amesema.
Kwa upande mwingine amehimiza vijana kufanya kazi kwa kuwa ni agizo la Mungu kwamba atabariki kazi ya mikono ya yule anayefanya.
“Kumezuka mtindo wa watu kutofanya kazi kwa kigezo kuwa wanasubiri miujiza ya baraka kwa kumiliki majumba,magari na mali mbalimbali jambo ambalo si kweli na hakuna muujiza wa aina hiyo na wale wanaohamasisha miujiza bila ya kuwataka watu wafanye kazi ni matapeli tu,” amesema.
Oktoba Mwaka huu kutafanyika Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.