Na Lucy Ngowi
WAJUMBE na Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa umakini, kuzingatia sheria wakati wanapotoa huduma kwa Walimu.
Mwenyekiti wa TSC, Profesa Masoud Muruke amesema hayo wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe wa Tume ya kuwajengea uwezo Wajumbe hao juu ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu yanayofanyika mkoani Morogoro.
Amesema lazima kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazingatiwa kikamilifu katika kufanya uamuzi unaohusu masuala ya utumishi wa walimu ili kuepuka kuwanyima walimu haki zao na kutoiingizia hasara Serikali pale walimu wanapokata rufaa kutokana na kutotendewa haki.
Amesema katika mafunzo hayo wajumbe wa TSC watapata uelewa wa kutosha hususan katika Mchakato wa kinidhamu, Rufaa kwa walimu na matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Tume.
Awali, Katibu wa TSC, Paulina Nkwama amesema kupitia mafunzo hayo ya siku mbili Wajumbe wa Tume watapitishwa kufahamu Majukumu ya Tume, mchakato wa kinidhamu na Rufaa kwa Walimu, Mfumo wa Kielectroniki wa Tume na Mada kuhusu Utunzaji wa Siri za Serikali.
Amesema kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu ni mojawapo ya Taasisi inayonufaika na Mradi wa kuimarisha Ujifunzaji na Ufundishaji katika Elimu ya Awali na Msingi (Mradi wa BOOST).
Amesema Mradi huo unatekelezwa kwa mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 500.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ni wa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2025/26.
Maelezo yake ni kwamba, katika muda wa utekelezaji tume hiyo ilitengewa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni mbili sawa na Sh. Bilioni 4.68.