Na Mwandishi Wetu
Mkutano wa 20 wa Kawaida wa Waratibu wa Kitaifa wa Nchi za Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) umefanyika, jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) na wa Wakuu wa Nchi na Serikali (SUMMIT) wa Jumuiya hiyo, utakaofanyika Novemba 13 na 15, 2025.
Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa DRC, Floribert Anzuluni Isiloketshi, amefungua mkutano huo na kuwataka waratibu hao kuwasilisha mapendekezo yatakayoboresha utendaji wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu ili iweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya msingi,
Ikiwemo kuimarisha amani, usalama na maendeleo katika nchi 12 wanachama wa Jumuiya hiyo.

Tanzania, ikiwa miongoni mwa waasisi wa ICGLR, inashiriki kikamilifu kupitia Mratibu wa Kitaifa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ellen Maduhu, ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania.
Katibu Mtendaji wa ICGLR, Balozi João Samuel Caholo, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake, bado zinahitajika jitihada zaidi kuhakikisha amani ya kudumu na usalama katika Ukanda huo, hususan katika DRC, Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ameeleza kuwa umasikini, ukosefu wa usawa na wananchi kutozifikia rasilimali za nchi zao ni miongoni mwa vyanzo vya migogoro barani Afrika, akisisitiza umuhimu wa kukomesha migogoro kwa kushughulikia mizizi yake.




