Na Lucy Lyatuu
CHAMA cha Wafanyakazi Wa Serikali Na Afya Tanzania (TUGHE) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamepongeza hatua ya serikali kupitisha sheria kuwa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa aliyejifungua mtoto njiti kujumuishwa kuwa wiki 40 za ujauzito.
Aidha sheria hiyo imepitisha baba kupewa nyongeza ya likizo ya uzazi kutoka siku tatu na kuwa siku saba kwa wafanyakazi waliojifungua mtoto njiti.
Pongezi hizo zimetolewa Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Tughe , Dk Jane Madete kwa kushirikiana na mtandao wa haki ya afya ya uzazi na taasisi ya Doris Mollel Foundation.
Akizungumza Madete amesema suala la nyongeza ya uzazi kwa wafanyakazi waliojifungua mtoto njiti lilikuwa ni maombi ya muda mrefu yaliyoasisiwa na Taasisi ya Doris Mollel Foundation tangu mwaka 2017 na baadae mwaka 2023 kuungana na mtandao wa haki ya afya pamoja na Tughe ili kuhakikisha suala hilo libakubalika.
Aidha amesema Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA ) lilibeba suala hilo na mwaka jana 2024 liliwakilishwa kwenye siku ya Wafanyakazi ambapo Januari 31,2025 serikali ilipitisha rasmi kuwa sheria.
“Kwa pamoja tumekuja kutoa pongezi za shukrani pamoja na Bunge la Jamhuri ya Tanzania kupitisha maombi hayo kuwa sheria kuanzia sasa, ” amesema.
Amesema akiwasilisha Bungeni maelezo ya Mswaada wa marekebisho ya sheria za kazi namba 13 wa mwaka 2024,Waziri wa Madini Anthony Mavunde kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi Ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete alieleza kuwa kuanzia sasa mfanyakazi atakayejifungua mtoto njiti likizo yake itaisha baada ya kufikisha wiki 40 ya ujauzito na baba kupewa siku saba za mapumziko.
Madete amesema kwa pamoja TUCTA, TUGHE na Taasisi ya Doris Mollel na Mtandao wa HakibYa Afya Ya Uzazi tunapongeza hatua hiyo kwani itasaidia kuimarisha ustawi wa mfanyakazi.
Amesema kabla ya sheria hiyo ilikuwa ni changamoto kwa mfanyakazi ikiwemo ya afya kwani wanahitaji muda mwingi wa kupumzika pia kuhudumia mtoto tangu kipindi cha uangalizi anaporuhusiwa kutoka hospitali.
“Mbali na changamoto hiyo ya kiafya pia wamekuwa wakipoteza ajira zao jambo linalosababisha kupata msongo wa mawazo hata kuathiri malezi ya mtoto aliyezaliwa, ‘ amesema.
Amesema kufuatia nyongeza hiyo ya likizo itasaidia wanawake hao kupata muda wa kutosha kuhudumia mtoto kwa kipindi chote bila kuwa na wasiwasi na kupoteza ajira.
Amesema na akiwa kazini afya itakuwa imara na kufanya kazi kwa tija hivyo wanaipongeza serikali kwa hatua hiyo.