Na Vincent Mpepo (OUT)
WANATAALUMA katika taasisi za elimu ya juu nchini wamehimizwa kubadili mtazamo wao kuhusu tafiti kwa kuzitumia kama nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni, badala ya kuziona kama hitaji la kitaaluma pekee la kukamilisha masomo.
Wito huo umetolewa lna washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya ushauri wa kitaalamu yanayoendelea katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), jijini Dar es Salaam, yakihusisha wanataaluma kutoka Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii pamoja na vitivo vingine.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mtiva wa Kitivo, Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii, Dkt. Mariana Makuu, amesema kuwa ni wakati wa wanataaluma kubadili mwelekeo kutoka tafiti za kinadharia kwenda kwenye tafiti zenye matokeo halisi kwa jamii.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza umahiri wa ushauri wa kitaalamu, hatua itakayosaidia kutatua changamoto za jamii, kuongeza mapato na kuimarisha taswira ya taasisi.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo, Innocent Deus, amesema kuwa tafiti zinapaswa kuelekezwa katika kutatua changamoto halisi za jamii ili kuongeza thamani ya taaluma na kuhalalisha mchango wa wanataaluma mbele ya wadau wa maendeleo.
Amesisitiza pia umuhimu wa ushirikiano kati ya wanataaluma na taasisi zenye uzoefu ili kuimarisha ubunifu na fursa za miradi.
Akichangia mjadala, Dkt. Janeth Laurean amependekeza kuwepo kwa utaratibu wa kuwatambua wanataaluma wabunifu watakaobuni tafiti zitakazoingizia chuo mapato.
Aidha, imebainika kuwa bado kuna mtazamo kwa baadhi ya wasomi wa kuiona elimu kama njia ya kuhitimu tu, badala ya chombo cha kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.



