Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WATUHUMIWA wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, kwa tuhuma za kufanya mauaji ya mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), aitwaye Amani Simbayao ikiwa ni pamoja na kumjeruhi Adriano Fredrick wa mamlaka hiyo.
Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Muliro ametaja watuhumiwa hao kuwa ni Deogratius Masawe (49) na Idd Bakari (30) wote wanafanya kazi ya ukuli wakazi wa Tegeta kwa Ndevu.
Wengine ni mpiga debe Omar Issa (47), mkazi wa Tegeta Dawasco na Rashid Mtongma (29) mwendesha Bodaboda mkazi wa Bunju.
Amesema watuhumiwa hao na wengine ambao bado wanahojiwa kwa kina walikamatwa baada ya kuwashambulia maofisa hao wa TRA wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisheria.
“Waliliharibu pia gari namba STL 9923 aina Toyota Land Cruiser Hardtop nyeupe mali ya Mamlaka ya Mapato Tanzania,” amesema.
Tukio hilo limetokea Disemba tano, 2024 majira ya saa tatu usiku eneo la Tegeta kwa Ndevu Kinondoni baada ya Maofisa hao wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kukamata gari namba T 529 DHZ aina ya BMW rangi nyeupe lililodaiwa kuwa na makosa ya kikodi.
“Jeshi la Polisi Kanda maaalum ya Dar es Salaam linawaonya vikali na halitavumilia watu ambao wanataka kujenga tabia ya kuwashambulia watumishi wa Serikali wakati wakitekeleza majukumu yao licha ya kuwa wanakuwa wamefuata taratibu zote za kisheria,” amesema.
Amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika kwa kuwafikisha kwenye mamlaka zingine za kisheria.