Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WANANCHI wametakiwa kutambua kuwa Katiba ya Tanzania hubeba masharti ya jumla kuhusu masuala mbalimbali ya nchi, lakini ufafanuzi wa kina hupatikana kupitia sheria, kanuni na miongozo mingine rasmi.
Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini, Onorius Njole, ameeleza hayo alipowasilisha mada kuhusu majukumu na mafanikio ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD), katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kilichofanyika jijini Dodoma.
Njole amesema baadhi ya malalamiko ya wananchi juu ya kunyimwa haki zao yanatokana na kutotambua kuwa Katiba haitoi haki hizo moja kwa moja bali huweka msingi wake, ambao unahitaji kusomwa sambamba na sheria husika.

Ametoa mfano wa haki ya kuishi iliyo kwenye Katiba, lakini sheria inaruhusu adhabu ya kifo kwa makosa ya jinai maalum.
Ameongeza kuwa haki ya kuchagua na kuchaguliwa, ambayo pia imo kwenye Katiba, hutekelezwa kwa kuzingatia sheria na miongozo ya Tume ya Uchaguzi.
“Ukifika kupiga kura saa mbili usiku, huwezi kusimama na Katiba kudai haki yako kuna utaratibu unaopaswa kuzingatiwa.” amesema.
Kwa msingi huo, amewataka wahariri na wanahabari kusaidia jamii kuelewa namna Katiba, sheria, na miongozo vinavyofanya kazi kwa pamoja ili kupunguza upotoshaji na sintofahamu kuhusu masuala ya kisheria.
Akielezea mafanikio ya Ofisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano, Njole amesema kuwa ofisi yake imekamilisha kazi ya urekebishaji wa sheria na kuchapisha Toleo la Mwaka 2023, kutafsiri sheria kuu 433 kati ya 446 kwa Kiswahili, na kufanya upekuzi wa mikataba 3,446 pamoja na hati za makubaliano 729.
Pia wameandaa sheria 68 na kutengeneza sheria ndogo 5,708.
Ameahidi ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na wanahabari katika kutoa ufafanuzi wa masuala ya kisheria ili kujenga uelewa wa pamoja na kusaidia taifa kufikia maendeleo kupitia utawala bora wa sheria.
Awali, akifungua kikao kazi hicho, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samweli Maneno amewataka wahariri kuhakikisha habari zinazohusu sheria zinatoka kwa mamlaka sahihi ili kuepusha upotoshaji wenye athari kwa taifa na jamii.
Maneno amesisitiza kuwa amani na umoja vinavyotokana na utawala wa sheria ni msingi wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2020.
Amesema pasipo amani, hakuna shughuli ya maendeleo itakayoweza kufanyika, hivyo ni muhimu kuzingatia haki, wajibu, na sheria zinazotuongoza.