Na Lucy Ngowi
GEITA: MAMIA ya wananchi wamefurika katika banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwenye Maonesho ya Nane ya Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, kwa ajili ya kupata majiko ya kisasa ya kupikia kwa bei nafuu.
Akiwa katika banda la REA, Mhandisi wa miradi kutoka REA, Evance Kabingo amesema katika banda hilo, REA inatoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na huduma za umeme vijijini.
Lengo likiwa kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni, na kuwaelekeza kwenye matumizi ya majiko ya gesi na majiko banifu yanayolinda afya na mazingira.

Kabingo amesema serikali imeamua kugharamia sehemu kubwa ya gharama za majiko hayo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuhamia kwenye nishati safi.
“Kwa sasa, majiko banifu yanauzwa kwa Sh 6,200 tu kutoka bei ya awali ya Sh 41,300. Serikali kupitia REA inagharamia asilimia 85 ya gharama. Kwa upande wa majiko ya gesi, wananchi wanachangia Sh 17,500 huku serikali ikichangia asilimia 65,” amesema Kabingo.
Katika maonesho hayo, majiko banifu 1,000 na mitungi ya gesi 500 vinatarajiwa kugawiwa kwa wananchi waliotimiza vigezo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuongeza matumizi ya nishati safi majumbani.
REA pia inatoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu athari za matumizi ya nishati chafu na faida za kutumia nishati safi, hasa katika maeneo ya migodi ambako uharibifu wa mazingira umekuwa mkubwa kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Amebainisha kuwa mradi mkubwa wa usambazaji umeme vijijini unatarajiwa kuanza mwezi ujao, na utahusisha usambazaji wa umeme katika vitongoji 9,009 nchini kote.
Lengo la REA ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, kila kijiji na kitongoji nchini kinakuwa kimefikiwa na huduma ya nishati ya uhakika.

Picha zote zimepigwa na Steven Nyamiti wa Wakala wa Nishati Vijijini ( REA)
Wananchi waliofaidika na majiko hayo wameeleza shukrani zao kwa serikali kutokana na msaada huo wa nishati safi.
Nasra Makungu, mkazi wa Geita, amesema, “Nimefanikiwa kupata jiko banifu kwa bei nafuu kabisa. Bila msaada wa serikali, isingekuwa rahisi kwetu. Tunashukuru kwa kutujali.”
Naye Peregia Paskali wa Nyamkunba amesema, “Majiko haya ni msaada mkubwa kwa familia zetu. Yatasaidia kupunguza gharama za kuni na kulinda afya zetu.”