Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Palamagamba Kabudi, amepongeza ubunifu wa kutoa vitabu kwa njia ya sauti, akisema teknolojia hiyo itawasaidia watu wasiopata muda wa kusoma vitabu.
Waziri Kabudi alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la Kampuni ya Uchapishaji Vitabu ya Mkuki na Nyota katika Maonesho ya 32 ya Kitaifa ya Vitabu Tanzania yanayoendelea Dar es Salaam.

Amesema wazo la vitabu vya sauti ni muhimu kwa kuwa msomaji anaweza kusikiliza popote alipo, Aidha, amesisitiza kuwa kwa kuanza na vitabu vya Shaaban Robert kutawavutia vijana wengi.
“Kwa kuanza na aina hii ya vitabu tunawarithisha watoto wetu utajiri mkubwa wa maarifa. Naamini Maktaba ya Taifa nayo itafikiria kuwa na vitabu vya sauti, jambo litakalowasaidia hata watu wenye uoni hafifu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota, Mkuki Bgoya, amesema kampuni hiyo inatengeneza vitabu vya sauti kwa kuvisoma na kuvipatia ladha kulingana na mahitaji ya kila kitabu.
Ameeleza kuwa wana platform ya mtandaoni iitwayo Digidigi Digital ambayo inawawezesha watu kusikiliza vitabu wakiwa katika mazingira mbalimbali kama vile wakiendesha gari au wakiwa nyumbani.
Pia, teknolojia hiyo inawanufaisha watu wasioweza kuona.
Bgoya amesema wameshaanza kurekodi mfululizo wa vitabu vya Shaaban Robert, vitabu vya viongozi, na vitabu vya watoto kama Hadithi za Katope.
Pia wameandaa vitabu vya sauti vya wasifu wa watu maarufu, na kazi hiyo inaendelea.
Hadi sasa, kampuni hiyo imerekodi vitabu 50 vya sauti, na inapanga kuwa na app maalumu ambayo watumiaji watalipia ada ya mwezi ili kusikiliza maudhui yote. Vitabu hivyo vimetayarishwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Aidha, wanatarajia kuwa na master classes, ambapo wataalumu mbalimbali watatoa mafunzo kuhusu mada tofauti kupitia mfumo huo.
Bgoya amesema teknolojia hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Januari 2026.

