Maji Kutiririka Kwa Uhakika Mwanza Kufikia Mwaka 2026
Na Lucy Ngowi
MWANZA: MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), imesema utekelezaji wa mradi mkubwa wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji wa maji safi jijini Mwanza umefikia zaidi ya asilimia 35 ya ukamilishaji.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa MWAUWASA, Vivian Temu, ameeleza hayo katika ziara ya waandishi wa habari ya kutembelea miradi hiyo.

Amesema ujenzi wa matenki matano ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni 31 unaendelea katika maeneo ya Kagera (lita milioni 10), Kisesa (milioni 5), Fumagila (milioni 10), Nyamazobe (milioni 5) na Usagara (milioni 1).
Amesema Mradi huo pia unahusisha ulazaji wa mtandao wa bomba wenye urefu wa kilomita 40.5, ambapo mpaka sasa KM 13.7 tayari zimeshalazwa kutoka katika vituo vya kusukuma maji vinavyojengwa maeneo ya Sahwa na Butimba kuelekea matenki husika.

“Mradi huu ni muhimu kwa maendeleo ya wakazi wa Mwanza. Tunatarajia kazi ya ulazaji wa bomba kuelekea tenki la Kisesa, ambalo ujenzi wake umekamilika, itakamilika mapema ifikapo Machi 2026,” amesema.
Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika rasmi Desemba 2026, na utakapokamilika, unakadiriwa kunufaisha zaidi ya wananchi 450,000 wa jiji la Mwanza na viunga vyake, hususan wakazi wa maeneo ya pembezoni na yale yenye miinuko mikali ambayo hapo awali yalikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji safi.
Amesema matenki yanayojengwa yamepangwa kupokea maji kutoka kwenye chanzo kipya cha uzalishaji maji cha Butimba, ambacho pia ni sehemu ya mradi huu unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD – Agence Française de Développement).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Waisa Werema, ambaye eneo lake limepitiwa na mradi huo, ameleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo akisema kuwa umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji katika jamii yao.
“Tunatoa pongezi kwa serikali na kwa Mkurugenzi wa MWAUWASA, Neli Msuya, kwa ushirikiano na viongozi wa mitaa katika kutatua changamoto pale zinapojitokeza,” amesema Werema.
Mradi huo una lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi, kuongeza uwezo wa hifadhi ya maji, na kupunguza uhaba wa maji kwa wakazi wa Mwanza, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza ustawi wa afya, uchumi na mazingira ya wakazi wa jiji hilo kwa ujumla.