Na Danson Kaijage
DODOMA: OFISA Mtendaji Mkuu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF),Peter Mwasalyanda amesema walimu wapatao 1585 wamepatiwa mafunzo juu ya umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Mwasalyanda amesema hayo leo alipokuwa akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO Jijini Dodoma.
Amesema jambo hilo la kuwapatia elimu hiyo ya TEHAMA ni hatua kubwa ya kuwawezeshe kutenda kazi zao kwa kujiamini na kwa uzoefu.
Amesema elimu hiyo kwa walimu itawawezesha pia kuvielewa vifaa vya TEHAMA hata pale vinaposumbua wasipate usumbufu wa kuwatafuta mafundi kwa mambo ambayo wanaweza kuyafanya wenyewe na kuwafundisha wanafunzi kwa uelewa zaidi.
Vile vile amesema kutokana na umuhimu wa elimu hiyo ya TEHAMA, mfuko huo umepeleka vifaa katika shule zenye uhitaji maalumu vyenye gharama ya Sh. Bilioni 1.8.
Kuhusu uboreshaji wa mawasiliano amesema, jumla ya minara 758 imejengwa kufikia Mei 12, mwaka huu 2025 inatarajiwa kuwa imekamilika.
Amesema kwa kipindi cha miaka minne minara 758 imejengwa, kati ya hiyo minara 430 tayari inatoa huduma.
Maelezo yake ni kwamba, minara hiyo itawahudumia watanzania milioni 8.5 ambapo serikali imewezesha ruzuku ya Sh. Bilioni 126.