Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kushirikiana na Kampuni ya YULHO kutoka Korea Kusini wanatarajia kujenga kituo kikubwa kitakachokuwa kinapima aina zote za madini zinazopatikana nchini.
Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Makamu Mkuu wa chuo, Proesa William Anangisye amesema kuwepo kwa kituo hicho kitakachogharimu zaidi ya Sh Bilioni 27 kitapunguza gharama ya kupeleka sampuli nje kwa ajili ya kupima.
“Uwepo wa kituo hiki kitaharakisha upatikanaji wa sampuli za madini ikiwa ni pamoja na kurahisisha mchakato mzima wa majibu ya vipimo,,” amesema.
Amesema pamoja na maabara itakayojengwa kituoni hapo pia kutakuwa na shule ya kufundisha wataalamu wa madini.
“Kituo hiki kitakuwa ni sehemu ya kichocheo cha kufanya utafiti zaidi kwa watanzania na kuongeza ujuzi,” amesema.
Kwa upande wake Rais wa Kampuni ya YULHO, Jae Seong Lee amesema lengo la kujenga kituo hicho nchini ni kusambaza teknolojia mpya za upimaji na utafutaji madini na kuongeza ajira kwa watanzania.
Naye Kaimu wa Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi, Dkt Abubakary Salama amesema kituo hicho kikkamilika kitakuwa na ajira ya zaidi watu 125 ambao 25 watatoka UDSM na zaidi ya 100 watakuwa nje ya chuo.
Amesema ujenzi huo unaanza mwaka huu wa fedha na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili.