Na Lucy Ngowi
CHUO Kikuu cha Dodoma ( UDOM), kimeshauri wananchi walime kisasa kwa kutumia njia ya ‘ Green House’ ili kupata mazao bora na kuongeza tija katika kilimo.
Ushauri huo umetolewa na Mtaalamu wa Maabara chuoni hapo, Julius Ngumba katika Maonesho yavWakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea Jijini Dodoma.
Ngumba amesema, imezoeleka mkoa wa Dodoma kuna ukame hivyo mazao hayawezi kustawi kutokana na hali hiyo, lakini UDOM ikafanya utafiti na kubaini teknolojia hiyo ya Green House inaleta matokeo chanya kwa maxao ya mbogamboga katika mkoa huo.
Amesema kwa kutumia teknolojia hiyo wameweza kulima mazao hayo ya mboga mboga kama nyanya, matango, karoti na soho ambazo zinastawi vizuri.
“Dodoma kuna uhitaji mkubwa wa vyakula lakini ni eneo ambalo jamii yake ina udumavu unaochangiwa na upungufu wa virutubisho katika jamii.
“Mboga zilikuwa haba kutokana na uhaba wa maji lakini utumiaji wa Green House unatatua changamoto hiyo,” amesema.
Amesema kwa kutumia teknolojia hiyo mazao ya mboga mboga yameweza kufanya vizuri.
Amesema jamii ya mkoa huo ikiamua kuachana na kilimo cha asili walichokizoea wataweza kuzalisha mazao bora kwa msimu wote kwa mwaka mzima.
” Siku zote kuhama njia asili kwenda mpya kuna gharama. Wakiweza kujenga watazalisha mazao bora msimu wote wa mwaka,” amesema.