Na Danson Kaijage
BAADHI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Mbabala, Jijini Dodoma, wameandamana hadi ofisi za CCM Wilaya wakieleza kutokuwa na imani na Diwani mteule wa kata hiyo, Pascazia Mayala.
Mmoja wa wanachama wa CCM, Donarld Mabala, amesema kuwa hatua ya CCM Wilaya kumrejesha diwani huyo ili agombee tena katika kura za maoni haijatenda haki kwa wanachama, kwani tangu achaguliwe miaka 10 iliyopita, hakuna maendeleo yoyote yaliyofanyika.

“Sisi wanachama wa CCM Kata ya Mbabala hatumtaki diwani ambaye amepitishwa tena kwenye kura za maoni. Tangu awe diwani hajawahi kuleta maendeleo yoyote. Badala yake, amekuwa mtu wa kusababisha migogoro isiyoisha, ikiwa ni pamoja na kuwapora wananchi ardhi yao,” amesema Mabala.
Naye mwanachama mwingine wa CCM, aliyejitambulisha kwa jina la Adela Chiwaligo, amesema diwani huyo amekuwa kikwazo kwa wakazi wa kata hiyo, kwa kushindwa kutatua matatizo ya wananchi.
“Sisi wana-CCM wa Kata ya Mbabala hatuna chuki naye kwa sababu ya nafasi au jinsia yake. Tatizo ni kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo wanayostahili.
“Kuna miradi mbalimbali ya maendeleo, kama mradi wa barabara ya mzunguko. Vijana wa hapa ndiyo waliopaswa kupewa ajira, lakini yeye huwachagua vijana anaowataka mwenyewe na kuwabagua watoto wetu,” amesema Adela.
“Jambo jingine ni kwamba, anapohitajika kukutana na wananchi kujadili masuala ya maendeleo, hututisha kwa lugha kali, jambo linalokwamisha maendeleo ya kata hii,” ameongeza.
Kwa upande wake, Pascazia Mayala alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, amesema hawezi kusema lolote kwa kuwa yeye ni mtoto wa CCM.
“Mimi siwezi kusema chochote kwa sababu mimi ni mtoto wa Chama Cha Mapinduzi, na chama ndicho kilichonipitisha kugombea nafasi ya udiwani. Kwa hiyo, waende wakamuulize aliyeniteua. Nitaendelea kuongoza. Waache wapige kelele, nitawanyoosha,” alisema Mayala.