Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: GAVANA wa Benki Kuu ( BOT), Emmanuel Tutuba amesema noti mpya za Tanzania zenye saini ya Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, pamoja na ya kwake, zinatarajiwa kuingia kwenye mzunguko Februari Mosi, mwaka huu.
Hayo ameyasema gavana Tutuba wakati akimkabidhi Waziri Nchemba, Noti kifani za Shilingi 10,000, 5000, 2000 na 1000 katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Amemweleza Waziri Nchemba kuwa kazi ya uchapaji upya wa noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, imekamilika.
Amesema wananchi wamejulishwa kupitia taarifa iliyotolewa kupitia Gazeti la Serikali.
Amesema noti hizo zitatumika sambamba na zilizopo hivi sasa, ambazo zina mwonekano wa zinazotumika hivi sasa zilizotolewa Mwaka 2010.
Ametaja mwonekano huo kuwa ni alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango imebadilishwa na kuwekwa Saini yako Dkt. Mwigulu Nchemba,
“Na Saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Profesa Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa Saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Emmanuel Tutuba,” amesema.
Naye Waziri Nchemba akizungumza
baada ya kupokea sampuli za Noti hizo mpya, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika.
Pia amempongeza Gavana Tutuba kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaendeleza heshima ya wataalam wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo yenye maslahi mapana kwa nchi yetu,” amesema.