Na Lucy Ngowi
DODOMA: MWAMKO wa ulipaji tozo kwa wakulima wanaotumia skimu za umwagiliaji katika maeneo tofauti nchini, umewezesha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupata sh bilioni mbili kwa mwaka 2024, ambazo zinaendeleza ujenzi mwingine.
Ofisa Kilimo Mwandamizi kutoka Tume ya Umwagiliaji, Lukombeso Udumbe ameeleza hayo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea jijini Dodoma.
Amesema Sheria ya Tume ya Mwaka 2013, namba nne, imeipa tume jukumu la kuhakikisha wakulima wakianza kuzalisha wanatoa tozo katika skimu ambazo uwekezaji umefanywa.
Amesema eneo hilo wamefanikiwa kulisimamia na kuwawezesha kupata kiasi hicho cha sh bilioni mbili kutoka sh milioni 150 kwa mwaka 2021/ 2023.
Amesema mbali na tozo hiyo, nusu ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kuanzia mwaka 2022/2023 na 2023/24 ilikwenda kwenye tume hiyo kwa ajili ya skimu za umwagiliaji.
Akizungumzia tozo hiyo ya wakulima, anaeleza kuwa kiasi kinachokusanywa kinaendeleza ujenzi wa miradi mingine ili sekta ya umwagiliaji iwe endelevu.
“Na hadi sasa tumeweza kuongeza eneo kubwa la umwagiliaji ukilinganisha na miaka ya nyuma. Kazi kubwa imefanyika ikiwa ni pamoja na kujenga mabwawa makubwa, lengo likiwa ni kuvuna maji ambayo yalikuwa yanapotea kwa kiasi kikubwa sana,” amesema.
Amesema kazi ya tume hiyo ni kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kuangalia maeneo ya wakulima na kuyafanyia tathmini kuangalia eneo husika kama linafaa.