Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imechukua hatua ya kudhibiti gugumaji vamizi la Kariba kwa kupeleka wadudu 4,252 katika Ziwa Victoria.
Aidha mayai ya wadudu hao yamepandikizwa kwenye ekari 15 za ziwa hilo, hatua inayolenga kudhibiti ueneaji wa mmea huo hatari.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya mamlaka kwa mwaka 2023/2024 hadi 2025/2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, amesema wadudu waliovunwa ni Mbawakavu wakubwa 3,231 na Viluwe luwe zaidi ya 1,021, kisha kusambazwa katika maeneo mbalimbali kuzunguka Ziwa Victoria.

Profesa Ndunguru amesema gugu la Kariba, lenye jina la kisayansi Salvinia molesta, ni mmea wa kigeni kutoka Brazil, na ripoti ya kwanza ya kuibuka kwa mmea huo Tanzania iliripotiwa Agosti 2024 katika Kivuko cha Busisi, Ziwa Victoria.
Wadudu waliosambazwa husaidia kudhibiti mmea huu vamizi katika maeneo ikiwemo Bwawa la Zungu, Wilaya ya Sengerema, Kijiji cha Rubungo na Bwawa la Nyitundu, Kata ya Kahumulo, Wilaya ya Misungwi.
Athari za gugu la Kariba: Gugu hili linaweza kuathiri vibaya wavuvi na wakulima wa maeneo yanayozunguka ziwa hilo kwa kuziba bwawa, kupunguza uingizaji wa mwanga na oksijeni ndani ya maji, na hivyo kuathiri uhai wa samaki na viumbe wengine wa majini.
Utafiti wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) unaeleza jinsi matope ya Salvinia yalivyoweza kupunguza oksijeni, kuongeza dioksidi ya kaboni, na kuathiri uzalishaji wa samaki na viumbe wengine wa maji.

