Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Author 10

TPDC Yaanza Majadiliano Kubadili Gesi Asilia Kuwa Kimiminika Ili Kufikishwa Nchi Nzima

Na Lucy Lyatuu,Dodoma
SHIRIKA La Maendeleo Ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza majadiliano na wawekezaji wa teknolojia ya kubadili gesi asilia kuwa kimiminika  hatua itakayowezesha gesi asilia kufikishwa nchi nzima.
Teknolojia ya Mini-LNG  imethibitika kibiashara kuweza kufikisha gesi asilia zaidi ya kilomita 500 kwa faida, ikisafirishwa kwenye malori maalum kufikia maeneo yasiyo na miundombinu ya mabomba.
Habari Picha 13755
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame amesema hayo  wakati akizungumza na waandishi wa habari  jijini humo kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo 2025/26 pamoja mafanikio ya Shirika hilo.
Amesema hadi sasa mazungumzo yanaendelea na Kampuni sita ambapo kati ya hizo tayari TPDC imesaini makubaliano ya mauziano ya gesi asilia na Kampuni tatu na tayari zinaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na kukamilisha ununuzi wa ardhi na Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kabla ya kutafuta Wakandarasi wa ujenzi.
Amesema upanuzi wa usambazaji wa Gesi Asilia kwa Viwanda, Majumbani, Taasisi na Magari katika mwaka wa fedha 2025/26, TPDC iliunganisha nyumba 1,000 katika mikoa ya Pwani na Lindi na kuunganisha viwanda viwili.
Amesema Shirika pia liliendelea kutoa huduma katika kituo chake cha CNG Mlimani  chini ya uendeshaji wa Kampuni ya GASCO.
Vile vile,  amesema Shirika liliunganisha vituo vitatu  vya CNG ambavyo vinamilikiwa na wawekezaji binafsi.
Aidha amesema TPDC inaendelea kupanua miundombinu ya gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara, huku ikiendelea na hatua mbalimbali za kufikisha huduma katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Habari Picha 13756
Amesema , Shirika kupitia mkandarasi wake nchini China, linaendelea na usanifu na uzalishaji wa vituo vya CNG-V na CNG-V Mobile Stations ambavyo vitaletwa nchini na kuwekwa katika mikoa tajwa.
“TPDC inaendelea na utafutaji wa mafuta katika Kitalu cha Eyasi-Wembere kinachohusisha maeneo yaliyopo katika mikoa ya Singida, Tabora, Simiyu, Arusha na Shinyanga,” amesema na kuongeza kuwa
Utafiti huo unajumuisha uchukuaji wa taarifa za mitetemo kwa mfumo wa 2D na ni sehemu ya jitihada za kutafuta rasilimali mpya za mafuta nchini.
Makame ameongeza kuwa TPDC imekamilisha uchukuaji wa kilomita za urefu 779 na inaendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi yenye urefu wa kilomita 325.7. Awamu hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha, na jumla ya mradi utagharimu kiasi cha sh bilioni 53.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.