Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imetenga Sh. Bilioni 10 kwa kipindi cha miaka miwili ya fedha kuanzia 2025/2026 hadi 2026/2027, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya amali katika shule mbalimbali za sekondari nchini.
Uwekezaji huo unalenga kuunga mkono utekelezaji wa mitaala inayowapatia wanafunzi maarifa, ujuzi na stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira, pamoja na kuwawezesha kutumia wanachojifunza shuleni katika kujiajiri na kuajiriwa.

Meneja wa Miradi ya Elimu wa TEA, Mwafatma Mohamed, amesema hayo wakati akieleza mchango wa Mamlaka katika utekelezaji wa mitaala mipya mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, aliyetembelea banda la TEA katika Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (ACA), jijini Dar es Salaam.
Mohamed amesema TEA imeweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu na upatikanaji wa vifaa vya mafunzo ya amali ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kujenga stadi zinazohitajika katika maisha na soko la ajira.
“Katika kipindi cha miaka miwili ya fedha, tumetenga Sh. Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya amali katika shule mbalimbali za sekondari nchini,” amesema.

Aidha, amesema TEA imetenga Sh. Bilioni 4.1 kuboresha mazingira ya kujifunzia kupitia utekelezaji wa mpango wa Makundi Rika Mawili.
Kongamano hilo la siku nne lililoanza Septemba 22, 2026, linajadili mageuzi ya mifumo ya elimu Afrika, maboresho ya mitaala, maandalizi ya walimu na ubunifu katika zama za Akili Unde (AI) na teknolojia zinazoibuka.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!