Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imezindua Mkakati wa Taifa wa Usimamizi na Uendelezaji wa Mikoko 2025–2035, ikiwa ni hatua madhubuti ya kulinda, kurejesha na kutumia kwa tija rasilimali hiyo muhimu ya mazingira.
Zaidi ya Sh bilioni 54 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji Wa mkakati huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, ametoa rai kwa taasisi za serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha mkakati huo unatekelezwa kwa kasi, kwa ushirikiano mpana, na kwa kuleta matokeo dhahiri.
“Mikoko ni uti wa mgongo wa uhai wa Bahari ya Hindi. Huchuja taka, huzuia mmomonyoko wa fukwe, ni hifadhi ya kaboni, na ni mazalia ya samaki. Kuiacha iharibiwe ni kuhatarisha maisha ya watu na viumbe,” amesema Waziri Chana mbele ya viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Amebainisha kuwa Tanzania ina zaidi ya hekta 158,100 za mikoko zinazosambaa katika wilaya 14 za ukanda wa pwani.
Hata hivyo amesema, rasilimali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uvamizi wa maeneo, ujenzi holela, uchimbaji wa mchanga na uchafuzi wa mazingira.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, amesisitiza taasisi husika zichukue hatua mahsusi ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kushirikiana na mamlaka nyingine katika kulinda na kusimamia mikoko na taasisi za utafiti kufanya tafiti zenye mwelekeo wa matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.
Vilevile ameielekeza Wizara kushirikiana na sekta ya utalii kubadilisha mikoko kuwa vivutio vya kiutalii; na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa msaada wa kifedha, kitaalamu na kiufundi ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati huo kwa ufanisi.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Benedict Wakulyamba, na Mkurugenzi wa Sera na Maendeleo, Abdallah Mvungi, ilielezwa kuwa mkakati huo unalenga kuhifadhi angalau asilimia 60 ya mikoko iliyoharibiwa ifikapo mwaka 2035, huku jamii zikipewa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika shughuli mbadala zenye tija.
Kwa upande wa TFS, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, amesema mkakati huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na wadau wa ndani na nje ya nchi, na ni nyenzo muhimu ya kulinda ardhi oevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kupitia mkakati huu, tutashirikiana na jamii, sekta binafsi na watafiti kuhakikisha mikoko inakuwa urithi hai wa taifa,” amesema Prof. Silayo.
Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru, Pamoja na wadau wengine wameupongeza mkakati huo kwa kuwa na mwelekeo wa kisayansi, jumuishi na unaolenga matokeo ya muda mrefu.
“Serikali imeonesha dhamira ya kweli ya kuhifadhi ardhi oevu na mikoko kama sehemu ya vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dkt. Ngusaru.
Mashirika mengine yaliyoshiriki na kutoa mchango wa kitaalamu, kifedha na wa kielimu ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Asilia (IUCN), Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Hifadhi za Baharini na Maeneo Tengefu (MPRU), Mtandao wa Uhifadhi wa Ukanda wa Pwani (Mwambao), Shirika la EarthLungs, pamoja na Wetlands International.