Na Mwandishi Wetu
DODOMA: CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimeendelea kuimarisha ushiriki wa makundi maalum ndani ya chama hicho kwa kuendesha semina maalum iliyowakutanisha wawakilishi wa wafanyakazi wenye ulemavu kutoka ngazi ya Mikoa na Taifa.
Rais wa Shìrikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa TALGWU, Tumaini Nyamhokya amefungua semina hiyo iliyofanyika jijini Dodoma.
Nyamhokya, amesema Kamati ya Wafanyakazi Wenye Ulemavu ni nguzo muhimu ndani ya chama, akibainisha kuwa mchango wake ni mkubwa katika kuhakikisha maslahi na sauti za wafanyakazi wenye ulemavu zinasikika ipasavyo.
Amesisitiza kuwa kukutana kwa wawakilishi hao si tukio la mara moja, bali ni sehemu ya mkakati endelevu wa TALGWU wa kuimarisha ushiriki, uwakilishi na usawa kwa makundi yote muhimu ndani ya chama.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Wandiba Ngocho, amesema semina hiyo imelenga kuwaongezea uelewa wawakilishi wa wafanyakazi wenye ulemavu kuhusu masuala muhimu yanayogusa moja kwa moja ustawi wao mahali pa kazi.
Amefafanua kuwa kupitia semina hiyo, washiriki wanapata fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wao katika kutetea haki, usalama na maslahi ya wafanyakazi wanaowawakilisha.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni elimu kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), pamoja na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi (OSHA), ikiwa ni jitihada za kuwawezesha wawakilishi hao kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi zaidi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki, Mwakilishi wa Wafanyakazi Wenye Ulemavu TALGWU Taifa, Josephine Shimula, ameushukuru uongozi wa chama hicho kwa kuandaa semina hiyo pamoja na kuendelea kutambua na kuwapa nafasi viongozi wa wafanyakazi wenye ulemavu ndani ya chama.
Amesema semina hiyo imewajengea uelewa mpana na kuahidi kuwa elimu waliyoipata itatumika ipasavyo kuwatumikia na kuwatetea wafanyakazi wenye ulemavu kwa ufanisi zaidi katika maeneo yao ya kazi.























