Na Lucy Lyatuu
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kinondoni, Dar es Salaam imepokea malalamiko 85 ambapo malalamiko 46 yalihusu rushwa an 35 hayakuhusu rushwa.
Mkuu wa TAKUKURU, Kinondoni, Christian Nyakizee amesema hayo jana Dar es salaam wakati akitoa taarifa kuhusu utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024.
Amesem kwa malalamiko ambayo hayakuhusu rushwa, walalamikaji wameshauriwa na majalada kufungwa na wengine wameelekezwa sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko yao.
Amesema kwa malalamiko yanayohusu rushwa majalada yanaendelea kushughulikiwa nay apo katika hatua mbalimbali.
Aidha Nyakizee amesema taasisi hiyo hufanya mifumo mbalimbali ili kubaini mianya ya rushwa katika maeneo ya kiutendaji ya ofisi,taasisi au idara na kudhibiti.
Amesema katika kipindi hicho wamefanya uchambuzi wa mifumo ya uondoshaji taka ngumu ngazi ya kaya na maeneo ya biashara katika Manispaa ya Kinondoni.
Ameitaja mifumo iliyofanyiwa uchambuzi kuwa ni usimamizi na ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (POS) katika manispaa ya Ubungo.
Amesema eneo lingine ni uwasilishaji wa michango mifuko ya hifadhi ya jamii katika Manispaa ya Ubungo na usomaji mita na Ankara za maji kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kwa wilaya ya Ubungo.