GEITA: TAKRIBANI wananchi 200 wamepatiwa ushauri wa kitabibu kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Mifupa na Tiba (MOI) katika maonesho ya Sekta ya madini yanayoendelea mkoani Geita.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mgongo kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI), Dkt. Kenneth Mgidange, amesema idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kupata ushauri wa kiafya kuhusu matatizo ya mifupa, ubongo, na mgongo katika banda la taasisi hiyo.
“Tumeona muitikio mkubwa wa wananchi, ambapo takribani watu 200 wamehudumiwa kwa siku kadhaa za maonesho haya. Wengi wao walihitaji ushauri wa kitaalamu, na baadhi tumewashauri kufanya vipimo zaidi katika hospitali zao za karibu,” amesema Dkt. Mgidange.
Ameeleza kuwa huduma zinazotolewa na MOI ni pamoja na upasuaji wa ubongo, kuondoa uvimbe kupitia njia ya pua, upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu madogo, na upasuaji wa magoti kwa teknolojia ya kisasa inayoongozwa na akili bandia.
Dkt. Mgidange amesema: “Huduma za MOI ni za kibingwa na hutolewa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu. Wananchi wa Geita na mikoa mingine wanahimizwa kufaidika nazo,”.
Aidha, wananchi wametakiwa kutumia mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao kabla ya kufika MOI, ili kupunguza msongamano na muda wa kusubiri huduma, hasa kwa wagonjwa wanaosafiri kutoka mikoa ya mbali kama Geita.
Taasisi ya MOI ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kwenye maonesho ya madini ya Geita kwa lengo la kutoa elimu ya afya na huduma kwa jamii, sambamba na kuwafikishia wananchi huduma za kibingwa nje ya Dar es Salaam.