Na Richard Mrusha
WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inatarajia kufanya onesho la nane lijulikanalo kama Swahili International Tourism Expo (SITE) litakalofanyika Oktoba 11 hadi 13 , mwaka huu Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru amesema hayo leo Septemba 12, 2024 alipozungumza na Waandishi wa Habari.
Mafuru amesema lengo la onesho hilo ni kuwakutanisha watoa huduma waliopo katika mnyororo wa thamani wa Utalii ndani na nje ya nchi ambao watapata fursa ya kuonesha bidhaa zao za Utalii na kutengeneza Mtandao wa Biashara.

“Onesho la S!TE linaenda sambamba na Utekelezaji wa sera ya Taifa ya Utalii ya Mwaka 1999 pamoja na mkakati wa kutangaza Utalii Kimataifa ( 2020-2025 ) ambayo imetilia mkazo kutangaza Tanzania kama kivutiok Bora Cha Utalii Duniani.
“Onesho hili pia ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano lll ambapo zao la Utalii wa Mikutano na Matukio limeainishwa kama zao la Utalii la kimkakati kwa lengo la kufikia watalii milioni tano na mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo Mwaka 2025,” amesema.
Amesema Onesho hilo la nane la S!TE limebeba ujumbe usemao ” Explore Tanzania for a Life Time Investment and Seamless Tourism Experience” litahudhuriwa na waoneshaji wa bidhaa na huduma za Utalii zaidi ya 120.
Pia wanunuzi wa bidhaa na huduma za Utalii takribani 120 kutoka Nchi ambazo ni masoko ya Kimkakati ya Utalii wetu ikiwemo Ulaya, Asia na Amerika.
Kwa upande mwingine amesema onesho hilo litafuatiwa na ziara za mafunzo ambazo zinalenga kuwajengea uelewa wahudumu wa bidhaa za Utalii kuhusu vivutio vya Utalii vilivyopo Tanzania ili waweze kuvitangaza katika Nchi zao na dunia kwa ujumla.

” Mwaka huu ziara hizo zimejikita katika kufungua Kanda za Utalii zinazochipukia ikiwemo ukanda wa Utalii Magharibi na Ukanda wa Utalii Kusini, kufungamanisha shughuli za Utalii zinazofanyika Zanzibar na Tanzania Bara,” amesema.
Amewataka watanzania na Vyombo vya Habari kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na kutangaza onesho la S!TE 2024 kwa lengo la kuwafikia Wadau wengi zaidi Ndani na nje ya Nchi ili waweze kunufaika na fursa za onesho hilo.