Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: SHULE tatu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam zimenufaika na mafunzo ya kuendeleza ujuzi yajulikanayo kama ‘‘Skills for their Future’’ kupitia mradi wa TEHAMA.
Kaimu Meneja wa Usimamizi Miradi ya Elimu Tanzania (TEA), Mwafatma Mohamed ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), amesema programu hiyo ni ya kipekee katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Amesema mamlaka hiyo inajivunia ushirikiano na BRAC Maendeleo Tanzania katika juhudi za kuboresha elimu na maendeleo ya taifa.

Amesema Februari 2022, mamlaka hiyo ilisaini makubaliano maalum ya ushirikiano na Shirika la BRAC – Maendeleo Tanzania ambalo ni mdau muhimu wa maendeleo katika Sekta ya Elimu hapa nchini.
Amesema kupitia ushirikiano huo, jumla ya Kompyuta 60 na Vishkwambi 60 vyenye thamani ya sh. Milioni 132.6 zilitolewa kwenye shule tatu za Sekondari za Wilayani Temeke.
Amesema program hiyo imelenga kuwajengea walimu pamoja na wanafunzi uwezo wa kutumia TEHAMA katika Shughuli zao mbalimbali ikiwemo shughuli za kitaaluma pamoja na bunifu kwa kuwanufaisha wanafunzi 1,922 na walimu 64
Akizungumza kwa niaba ya shule nufaika Mkuu wa Shule ya Wailes Mwalimu Daudi Kassenga amesema, mradi huo wa TEHAMA umekuwa na manufaa makubwa kwa walimu pamoja na wanafunzi kitaaluma kwani umewasaidia kubuni njia mbalimbali za kufundisha na kuandaa masomo kiurahisi.

‘‘Kabla ya huu mradi, shule zetu za sekondari zilikuwa hazina Kompyuta wala maktaba, lakini kupitia mradi huu, kila shule imepata Kompyuta 20, vishkwambi 20 na kukarabatiwa chumba kimoja cha kuhifadhia vifaa hivyo vya TEHAMA,” amesema.
Anuary Josephati mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari Miburani amesema, amefaidika na mradi huo kwani wakati programu ya mafunzo inaanza alikuwa kidato cha kwanza.
‘‘Mimi nilikuwa kidato cha kwanza wakati mafunzo yanaanza hivyo nilijiwekea nadhiri kwamba lazima nisome na hadi sasa nimejifunza kubuni na kutengeneza mifumo mbalimbali inayoweza kutumika kurahisha kazi kwenye jamii lakini pia nimejifunza ujasiriamali kupitia TEHAMA,” amesema.
Kwa upande wa mwakilishi wa Mkurugenzi wa BRAC – Maendeleo Tanzania, Kalunde Simba amesema tafiti zinaonyesha changamoto ya wanawake na wasichana wanaojihusisha na masuala ya TEHAMA inachangiwa na ukosefu wa miundombinu ya kutosha na pia ujuzi mdogo wa walimu kuweza kutoa mafunzo husika kwa wanafunzi.
Naye Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Temeke, Niconia Amos amewapongeza TEA na BRAC Maendeleo Tanzania kwa kutekeleza na kufanikisha mradi huo kwani umekuwa chachu ya maendeleo kwa wanafunzi, hususan wasichana balehe na wanawake vijana