Na Mwandishi Wetu, Gulwe
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ameshauri kujengwa kwa mabwawa ya kisasa katika maeneo ya milimani ya vijiji vya Iyenge, Ludi, Vibewele na Mzogole wilayani Mpwapwa ili kudhibiti athari za mafuriko yanayosababisha uharibifu wa reli ya kati na makazi ya wananchi.
Simbachawene, ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe, ametoa ushauri huo wakati wa ziara ya Dkt. Mwigulu Nchemba katika kijiji cha Gulwe kukagua uharibifu wa miundombinu ya reli na makazi uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Amesema mabwawa mengi yaliyopo yalijengwa kwa teknolojia ya zamani, hivyo kuna haja ya kujenga mabwawa ya kisasa kwenye milimani ambako maji yanatoka ili kuyazuia yasishuke kwa wingi hadi maeneo ya chini.
Amesisitiza wataalamu wahusishwe kubuni mifumo itakayopunguza mtiririko wa maji kutoka milimani kwa kuyahifadhi kwenye mabwawa.
Aidha, ameshauri kujengwa kwa kituo cha afya kitakachohudumia wakazi wa eneo hilo pamoja na abiria wanaokwama safari reli inapoharibika.
Kwa upande wake, Dkt. Nchemba ameagiza TANROADS kufanya makadirio ya dharura kubaini gharama za ukarabati wa daraja la Godegode na korongo la Gulwe ili miundombinu irejee kupitika.
Pia amewahimiza wananchi kutunza mazingira kwa kuepuka ujenzi kwenye mikondo ya maji, ukataji miti holela na kilimo kisichozuia mmomonyoko wa udongo.
Akizungumzia barabara ya Mpwapwa–Gulwe, amesema mkandarasi tayari amepatikana na kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema serikali imetoa Sh. Bilioni 64 kurekebisha maeneo yaliyoathiriwa na mvua, yakiwemo Mtanana na Fufu.

