Na Lucy Lyatuu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ameliagiza Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) kuandaaa mpango utakaowezesha ujenzi wa Viwanda vidogo 20 Kwa Kila mkoa Kwa kuwa ,jambo hilo litasaidia kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira nchini.
Amesema lengo la mpango huo ni kuongeza thamani katika Viwanda na mpango huo uwe na matarajio ya kuzinduliwa kati ya 2025 hadi 2030 Ili kujibu matatizo ya wananchi.
Waziri Dkt. Selemani Jafo amesema hayo Dar es salaam alipotembelea Shirika la SIDO Kwa ajili ya kujitambulisha na kusalimia.
Amesema katika kupambana na tatizo la ajira nchini, huku vijana wengi wakihitimu masomo yao ni muhimu kwa Shirika Hilo kuhakikisha linawezesha ujenzi wa viwanda mbalimbali katika Kila mkoa jambo litakalopunguza tatizo la ajira nchini
“Kila mwaka vijana zaidi ya 64,000 huhitimu kozi mbalimbali na serikali haiwezi kuajiri wote na eneo kubwa linalotegemewa ni viwanda na Biashara,” amesema na kulitaka Shirika Hilo kupanga mpango wa miaka sita kuanzia 2025-2030 Ili kuwa na viwanda nchini.
Kadhalika amesema chini ya mpango huo, kila mwaka na Kila mkoa kuhakikisha viwanda vitatu vyenye Hadhi vinajengwa na ujenzi wa viwanda vya kati vipatavyo vitano.
Amesema mpango huo wa ujenzi wa viwanda utasaidia ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi.
Waziri Jafo amesema pamoja na mpango huo, Kila mkoa uwe na kongani ya kibiashara lengo likiwa ni Kila mkoa kushindana kibiashara.
‘ Katika hili la kongani, watu waangalie mahitaji na fursa ,zilizopo kwenye maeneo yao,” amesema Jafo na kuongeza kuwa kipindi hiki ni Kwa ajili ya kufungua mikanda na kuwa na mageuzi makubwa kwenye viwanda.
Aidha aliagiza Shirika Hilo kutoa taarifa ya maeneo yote ya wazi wanayo miliki na kubainisha shughuli zinazofanyika na kama yana tija kwa Shirika Hilo na kama sio ushauri utolewe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji amesema wamejipanga kwenda kutekeleza agizo la ujenzi wa viwanda 20 Kila mkoa na kuwataka wananchi kununua bidhaa zinazozalishwa nchini Ili kukuza viwanda hivyo.