Na Lucy Lyatuu
SERIKALI imesema Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa umewezesha migogoro ya ndoa iliyotatuliwa imeongezeka kutoka migogoro 12,068 kwa mwaka 2022 hadi migogoro 100,464 June, 2025.
Imesema imeendelea na jitihada za kuimarisha taasisi ya familia na ndoa kupitia Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa wa mwaka 2023.
Waziri wa Wizara Ya Maendeleo Ya Jamii, Jinsia Wanawake Na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima amesema hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia utekelezaji wa shughuli za maendeleo mbalimbali kwa makundi maalum kwa mwaka 2025/26 katika mkutano ulioandaliwa na Idara ya Habari Maelezo.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau hususani Vikundi vya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jami (SMAUJATA), Sauti ya Watoto Tanzania (SAWATA), Malezi Bora Network na LEMACHU vimeweza kuibua, kukemea na kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya ukatili.
Aidha, amesema tangu kuanzishwa kwa kampeni hizo jumla ya matukio 799 yameripotiwa na kushughulikiwa.
Dkt Gwajima amesema Serikali inaendelea kutoa huduma ya Malezi ya Kambo na Kuasili kwa ajili ya watoto waliokosa malezi katika ngazi ya familia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo vya Wazazi, Watoto kutupwa pamoja na kutelekezwa na Wazazi/Walezi.
Amesema takwimu zinaonesha huduma ya malezi ya kambo na kuasili imeongezeka kutoka Watoto 85 (Wavulana 45 na Wasichana 40) mwaka 2022 hadi kufikia watoto 562 (wavulana 279 na wasichana 283) mwaka 2025.
Ametoa wito kwa familia zenye uhitaji wa kutoa huduma ya malezi ya kambo na kuasili kuwasilisha maombi yao kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii kupitia Halmashauri zao.
Kuhusu uwezeshaji kwa wananchi amesema wananchi wanawezeshwa kiuchumi ili kuweza kujiajiri na kujipatia kipato kupitia fursa zilizopo, Serikali inafanya juhudi mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo kutoa Mikopo yenye Masharti Nafuu kwa Wafanyabiashara Ndogondogo ambao idadi kubwa ni vijana ili kuwawezesha kuimarisha mitaji, kukuza biashara na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Ameseme uwezeshaji huo unatekelezwa kupitia Benki ya NMB, inayosimamia utoaji, usimamizi, na urejeshaji wa mikopo hiyo yenye riba ya asilimia saba .
Amesema Kupitia Mikopo hiyo jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 4,870 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya Sh 9,938,820,000.
Ametoa rai kwa wafanyabiashara ndogondogo kujitokeza na kusajiliwa kwenye mfumo wa Wafanyabiashara Ndogondogo Management Information System (WBN kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri zao.
Aidha Dkt Gwajima amehimiza jamii kutambua kuwa amani ni msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo, kukosekana kwa amani kunasababisha athari hasi hasa kwa makundi maalum yakiwemo Wazee, Wanawake na Watoto.
Amezitaja athari hizo ni pamoja na: kupotea na uharibifu wa mali na makazi; kuongezeka kwa watu wanaopata ulemavu; kutokea kwa vifo na magonjwa ya mlipuko; kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia; Kuongezeka kwa msongo wa mawazo na kiwewe; na kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii kama vile huduma za afya, maji safi na salama, usafiri, umeme na chakula.
Amesema Wizara yake imeanzisha utaratibu kutoa huduma bora zaidi kwa jamii kupitia falsafa mpya ya KAZA KAZAWA (Kasi zaidi, Karibu zaidi na Wananchi).

