Vituo vya Afya Vyapanda kwa Asilimia 71
Na Danson Kaijage
DODOMA: MKOA wa Arusha umefanikiwa kukusanya na kutumia Sh. Trilioni 3.5 katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo kuboresha huduma za afya, miundombinu ya utawala na kuongeza pato la mwananchi.
Akizungumza jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO kuhusu mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, amesema hayo.

Amesema mkoa huo umepiga hatua kubwa hasa katika sekta ya afya ambapo jumla ya vituo vipya vya afya nane vimejengwa, na kufanya idadi kufikia vituo 66, huku zahanati mpya 38 zikiongezwa na kufikisha jumla ya 350.
“Serikali imetoa zaidi ya Sh. Bilioni 94.2 kwa ajili ya huduma za afya pekee, ambapo Bilioni 57.07 zilitumika kwenye ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya afya, na Bilioni 26 kwenye ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2021 hadi asilimia 93 mwaka 2025.
Amesema mashine za kisasa kama CT-Scan, ECHO, ECG na MAMOGRAPHY zimefungwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, hatua inayoboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa.
Pia amesema huduma mpya za kibingwa 11 zimeanzishwa ikiwemo upasuaji, magonjwa ya figo, uchunguzi wa saratani, afya ya mama na mtoto, pamoja na mfumo wa mkojo.
Amesema katika sekta ya utawala, Sh. Bilioni 958.7 zimetumika kujenga majengo ya kisasa katika Halmashauri za Monduli, Ngorongoro, na Arusha Jiji ambapo ujenzi unaendelea, sambamba na ukumbi na nyumba ya Mkuu wa Mkoa.

Vile vile amesema ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo umeongezeka hadi kufikia asilimia 84, huku pato la mwananchi likipanda kutoka Sh. Milioni 3.2 mwaka 2020 hadi Milioni 3.6 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 12.5.