Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema serikali inaendelea kutekeleza dhamira ya kuwalinda wafanyakazi ambao ni nguzo muhimu katika maendeleo ya Nchi.
Ridhiwani amesema hayo Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 10 ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), tangu kuanzishwa kwakwe, ikiwa ni hatua kubwa katika kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na familia zao.

Amesema WCF imeongeza wigo wa mafao ambapo hadi sasa unatoa jumla ya mafao saba ikiwemo Fao la Matibabu yasiyo na kikomo, Fao la Ulemavu wa Muda Mfupi, Fao la Ulemavu wa Kudumu, Fao la pensheni kwa wategemezi, Fao la Wasaidizi wa Mgonjwa, Fao la Utengamao na Fao la Msaada wa Mazishi.
Amesema WCF umeboresha mifumo ya ushughulikiaji wa fidia kwa wafanyakazi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 90 ya huduma zinazotolewa zinapatikana mtandaoni, hali ambayo imeongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wa mfuko.
Pia amesema mfuko huo umekuwa ukitoa elimu na uhamasishaji kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi na usalama kazini, hivyo wafanyakazi wengi kuelewa haki zao pale wanapopata ugonjwa ama ajali zinazotokana na kazi zao.

Kwa upande mwingine Waziri Ridhiwani amesaini kanuni zinazoanzisha fao jipya la Utengamao linalolenga kumsaidia kumrudisha mfanyakazi aliyeumia kazini katika hali ya kuweza kuzalisha na kuendeleza msingi bora wa maisha.
Ridhiwani ameishukuru menejimenti ya WCF kwa kuishi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwahakikishia watanzania kuendelea na uzalishaji hata baada ya kuumia kazini.
Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema mfuko huo umepewa cheti cha ithibati katika utoaji wa huduma bora kwa viwango vya Kimataifa Juni mwaka jana, 2024 hatua inayoongeza imani chanya kwa wadau wote wanaohusika kwenye mnyororo wa fidia kwa wafanyakazi nchini.