Na Lucy Ngowi
WAZIRI Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema wafanyakazi wasipokuwa na chombo kinachoelezea mambo yao, watakuwa hawajajitendea haki.
Aidha amepongeza kurejea kwa gazeti la Mfanyakazi TANZANIA, ambalo lilikuwepo zamani likafa kisha limerudi tena.
Ridhiwani amesema hayo kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), jijini Dodoma alipokuwa akizungumzia kuanza tena kuchapishwa kwa gazeti la Mfanyakazi TANZANIA ambalo siku za nyuma lilikuwepo.
Amesema sio tu kwa wafanyakazi kuwa na chombo chao cha habari, bali hata wale wasio wafanyakazi watanufaika kupitia chombo hicho kwa kupata taarifa zinazohusu maslahi ya wafanyakazi, na taarifa nyingine.
“Uzinduzi kwanza wa gazeti la Mfanyakazi ni jambo kubwa sana, mambo mengi yanafanyika katika nchi, wafanyakazi kama hawatakuwa na chombo kinachowaelezea mambo yao hata wasio wafanyakazi wakapata taarifa za maslahi ya wafanyakazi watakuwa hawajajitendea haki,” amesema Ridhiwani.
Amesema endapo vyombo vya habari vikitumika vizuri vina nguvu ya kuunganisha, vikitumika vibaya vitabomoa.
Akimkaribisha Waziri Ridhiwani katika Mkutano huo, Rais wa shirikisho hilo Tumaini Nyamhokya amesema gazeti hilo limerudi tena.
Pia amesema katika mkutano huo, waliazimia litoke toleo maalum la mkutano.
Amesisitiza kuwa gazeti hilo litakuwa linaendelea kutoka na kwamba matamanio yao wangependa litoke mara mbili kwa wiki.