Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAADHIMISHO ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), yanafanyika wakati Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kukamilishwa kwa ujenzi wa vyuo vya VETA vya hadhi ya Mkoa katika mikoa yote nchini ambayo haina vyuo hivyo.
Ikiwa ni pamoja na vyuo vyenye hadhi ya Kiwilaya katika wilaya zote ambazo havina vyuo hivyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo kilele chake kitaadhimishwa kwa siku nne kuanzia Machi 18 hadi 21, mkoani Dar es Salaam.
“Kwa maana hiyo sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa Chuo chenye hadhi ya Mkoa cha VETA kwa mkoa wa Songwe ambao hauna chuo cha VETA cha hadhi ya mkoa.
“Na tunaendelea na ujenzi wa vyuo 64 katika wilaya 64 ambazo hazina vyuo vya VETA kwa hiyo maadhimisho yanakuja kipindi ambacho Rais amepania kuhakikisha elimu hii ya ufundi na ufundi stadi inafikia vijana wote wa Tanzania wanaohitaji kwenda katika mafunzo haya,” amesema.