Na Lucy Ngowi
RAIS Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania(TPHPA), kwa kuiwezesha nchi kupata cheti cha kiwango cha kimataifa.
Samia ametoa pongezi hizo wakati akifungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma, Jijini Arusha.

“Haya yamewezekana kutokana na kuunganishwa kwaTaasisi ya Utafiti ya Viuatilifu vya Ukanda wa Kitropiki na Kitengo cha Huduma za Afya za Mimea, hivyo malengo yamekusanywa, wamefanya kazi moja, wamejielekeza kwenye ule mlengo waliotakiwa kufanya kazi.
“Sasa Tanzania ina viwango vya ubora vya kimataifa. Ambavyo kupata ubora wa kimataifa umenyanyayua Tanzania kama nchi lakini pia kazi zetu sasa zinaenda kutambuliwa kimataifa.
“Masoko hayatatukimbia ya kimataifa lakini zaidi ya hayo wameweza kukusanya fedha na wanatoa gawio serikalini,” amesema.
Rais Samia amesema hiyo ndiyo faida ya kuchanganya taasisi ambazo hazifanyi vizuri kutokana na malengo kujirudia au kupitwa na wakati.
Amesema mifano aliyoitoa ni mafanikio ya kipindi kifupi cha mamlaka hiyo kuundwa baada ya kuunganishwa zilizokuwepo.
Hivi karibuni kampuni na taasisi zilitoa gawio serikalini ambapo TPHPA ilifanikiwa kutoa sh bilion 3.7.

Maelezo ya Profesa Joseph Ndunguru, gawio hilo la sh 3.7 limeifanya mamlaka hiyo kuwa ya kwanza katika kundi la taasisi zilizotoa gawio kubwa kwa mara ya kwanza.
Profesa Ndunguru amesema awali mamlaka hiyo ilitarajiwa kutoa gawio la sh milion 968, lakini makusanyo ya mwaka wa fedha 2023/ 2024 yamewezesha kufikia kiwango hicho cha sh bilioni 3.7.
Amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 mamlaka hiyo ilikasimua kukusanya kiasi cha fedha cha sh bilion 6.4 mapato ya ndani.
“Lakini kufikia Mei 31 mwaka huu mamlaka imeweza kukusanya sh bilioni 19. 9 ya makadirio ya makusanyo ya mwaka mzima kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya mapato ya ndani,” amesema.
Amesema makusanyo hayo yameweza kuongeza kiasi cha gawio lake kwa serikali kuu kutoka sh milioni 968 hadi kufikia sh bilion 3.7.