Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imeagizwa kuhakikisha waandishi wa habari wote wanazingatia sheria, kanuni na miongozi inayosimamia taaluma yao ili kudhibiti uandishi usio wa kimaadili na kuongeza heshima ya taaluma hiyo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi ameagiza hayo leo Machi 3, 2025 wakati akizindua bodi hiyo mkoani Dar es Salaam.
Kabudi amesema, “Katika hili tunapaswa kuanza kwa kuwalea na kuwapa miongozo mbalimbali juu ya taaluma yao,”.
Agizo lingine aliloagiza bodi hiyo ni kuandaa na kusimamia utaratibu wa usajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma, mfumo ambao unapaswa kuwa shirikishi na unaoendana na maendeleo ya teknolojia na mazingira ya sasa ya sekta ya habari.
Agizo lingine alilollitoa Profesa Kabudi kwa bodi hiyo ni kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma kwa kutoa miongozo na mafunzo ya mara kwa mara.
Ameiagiza bodi hiyo kushirikiana na vyombo vya habari, vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari, na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanapata mafunzo ya mara kwa mara na kuwa na ujuzi wa kisasa.
Pia ameiagiza kutoa elimu kwa wananchi ili waelewe umuhimu wa ithibati ya waandishi wa habari na jinsi inavyosaidia kuboresha sekta ya habari.
“Katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali, Bodi hii inapaswa kusaidia kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanatumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili. Hii ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika utoaji wa habari.
“Ikiwa ni pamoja na kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa usalama bila vitisho, unyanyasaji, au vikwazo visivyo vya lazima. Usalama wa wanahabari ni msingi wa uhuru wa vyombo vya habari,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando amesema bodi hiyo ni chombo muhimu cha kuhakikisha taaluma ya habari inafuata weledi na ubora unaotakiwa.
Amesema atatekeleza maagizo yote waliyopewa na Waziri Kabudi kwa moyo wa uzalendo, uaminifu na uadilifu.