Na Lucy Ngowi
RUKWA: MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), taasisi nunuzi na halmashauri kuhakikisha usajili wa vikundi vya vijana unaambatana na upatikanaji wa zabuni ili kuwawezesha kunufaika na fursa za kiuchumi.
Akizungumza Oktoba 14, 2026, katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye Uwanja wa CCM Nelson Mandela, Sumbawanga, mkoani Rukwa, amesema usajili pekee hautoshi bila vijana kupata zabuni na ujuzi wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Amesema Serikali inaendelea kuwawezesha vijana kupitia mitaji, mikopo ya halmashauri na programu ya Sh bilioni 200, akisisitiza fedha hizo ziwafikie walengwa na kuleta matokeo yanayopimika katika ajira na kujiajiri.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Joel Nanauka, amesema kampeni ya Mwenge wa Uhuru imeongeza usajili wa vikundi vya makundi maalumu katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
Amesema vikundi viliongezeka kutoka 1,556 vilivyosajiliwa kati ya mwaka 2023 na Machi 2026 hadi 33,524 kufikia Oktoba 2026.
Kati ya vikundi hivyo, 16,582 ni vya vijana, 15,412 vya wanawake, 789 vya wazee na 741 vya watu wenye ulemavu.
Nanauka amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, mikataba 205 yenye thamani ya Sh bilioni 25.076 ilikuwa imetolewa kwa makundi maalumu.
Ameeleza kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023 inazitaka taasisi kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa makundi maalumu yaliyosajiliwa NeST.
Aidha, amesema Mwenge wa Uhuru unaendeleza uanzishwaji wa majukwaa ya vijana yatakayowapa nafasi ya kueleza changamoto zao na kushiriki kutafuta suluhisho.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!