Na Lucy Lyatuu
KIKOSI Cha Usalama barabarani kimeahidi kuwasiliana na mkuu wa kituo cha polisi, eneo la Buguruni, Dar es Salaam ili kujua ni kwanini wanaona vijana wakichuja mafuta kwenye malori na mifuko bila kuchukua hatua.
Ahadi hiyo imetokana na malalamiko yaliyowasilishwa katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wamiliki wa malori wadogo na wa k ati Tanzania (TAMSTOA) ukishirikisha wadau mbalimbali wa uchukuzi.
Aidha Mkaguzi wa Polisi, kutoka kikosi hicho, makao makuu, Dumu Mwalugenge amesema ni wajibu wa raia pia kuchukua hatua pindi akiona kosa linatendeka .
Amesema kwa askari katika eneo hilo kuona raia wakichuja mafuta kwenye malori na kuacha kuchukua hatua sio jambo jema lakini atafuatilia kujua zaidi.
“Sio kila kosa linapofanyika askari wanakuwepo kwenye eneo husika, lakini kama mmekiri kuona vitendo vya vijana kuchuja mafuta kwa kutumia mifuko na askari kuona bila kuchukua hatua hilo litafuatiliwa na kupatiwa ufumbuzi,” amesema Mwalugenge.
Amesema askari wanaokuwa katika eneo hilo ni wazi kuwa wanatambua wajibu wao na majukumu yao.
Kuhusu bidhaa za hatari kama kama visu na mapanga kuuzwa hadharani amesema ni muhimu kwa wauzaji kuweka ndani ya ala jabla ya kwenda kwa mteja.
Akiwasilisha malalamiko yake, msafirishaji wa malori,Khalid Karwani alihoji uhalali wa vijana wanaochuja mafuta kwenye malori hususani eneo la Buguruni huku askari wakiona bila kuchukua hatua.
Kadhalika alihoji suala la bidhaa hatari kama vis una panga kuuzwa kiholela hadharani jambo ambalo ni hatari kwani linaweza kusababisha madhara kwa namna moja hadi nyingine.