Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendesha msako maalum kuanzia Agosti 18 hadi 25, mwaka huu 2025, na kukamata magari 15 yaliyokuwa yakiendeshwa bila namba rasmi za usajili.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari.

“Magari haya yalikuwa na namba bandia za usajili aina ya SSH 2530, kinyume na Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.
“Kuendesha chombo cha moto bila usajili rasmi ni kosa kubwa linalohatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara,” amesema Kamanda Muliro.
Katika hatua nyingine ya kuhakikisha usalama wa raia na kupambana na biashara haramu, Kamanda Muliro amesema mnamo Agosti 11, 2025, alikamatwa Ramadhani Makala, mkazi wa Tabata, kwa tuhuma za kusafirisha magunia ya mchele yaliyochanganywa na mizigo ya bangi.

“Tulimkamata mtuhumiwa akiwa anatumia gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T.733 AGT kusafirisha magunia 13 ya bangi yenye uzito wa takribani kilo 239 kutoka Morogoro kuelekea Dar es Salaam.
“Mizigo hiyo ilikuwa imefichwa kati ya magunia ya mchele kwa lengo la kudanganya vyombo vya usalama,” amesema Kamanda Muliro.
Aidha, kati ya Agosti 12 hadi 20, 2025, Jeshi la Polisi pia liliwakamata watuhumiwa wawili waliokuwa wakijihusisha na wizi wa mali mbalimbali za pikipiki. Watuhumiwa hao ni Hassan Hamis, mkazi wa Candle, na Elia Mapunda, mkazi wa Goba Njia Nne.
“Watuhumiwa walikamatwa wakiwa na vipuli vya pikipiki pamoja na pikipiki sita, mali zinazodhaniwa kuwa za wizi. Upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima unaohusika na wizi wa pikipiki jijini Dar es Salaam,” amesema.
Kamanda Muliro amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa, huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu au viashiria vyake mapema.
Jeshi la Polisi limeeleza dhamira yake ya kuendeleza misako na doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya jiji ili kudhibiti uhalifu, na kuhakikisha sheria inafuatwa kikamilifu na kila mwananchi kwa ustawi wa taifa.