Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema ni lazima jitihada za kuwekeza katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ziongezwe ili mwaka ujao Kongamano la sayansi liwe kubwa zaidi.
Profesa Mkenda amesema hayo wakati wa kufunga Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia na ubunifu, lililomalizika mkoani Dar es Salaam.
“Hili kongamano lazima tuendelee kuli ‘Support’ na liwe kubwa zaidi, na kwa maana hiyo lazima tuongeze jitihada za kuwekeza katika sayansi na teknolojia.

“Na kwa maana hiyo lazima tuhakikishe kwamba vijana wanaposoma sayansi itawasaidia, tunafanya upendeleo katika utoaji wa mikopo kwenye nasomo ya sayansi hatutakiwi tuchoke.
” Inatulazimu tusomeshe watu wengi zaidi nje katika maeneo ya sayansi,” amesema.
Katika hatua nyingine amesema serikali inaziangalia bunifu kwa karibu kuhakikisha zinasonga mbele kwa kuingia sokoni, tofauti na hapo haitasaidia.
” Hatuwezi kuona wana saayansi kama wanakaa katika mlingoti wa pembe za ndovu, kwamba wanafanya. Vitu ambavyo havitumiki kwa watu.
” Kwamba wasomi wanajifungia wanafanya mambo, wanapandishana vyeo kwa kufanya vitu vizuri lakini hawagusi maisha, ” amesema.
Amesema walichokiona katika kongamano hilo la tisa la sayansi ni mchango mkubwa kutoka kwa wanasayansi.