Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “MABADILIKO ya tabia nchi yapo, na mabadiliko yanaathiri walishaji wa mazao. Pia yanachangia uwepo wa visumbufu kwa maana magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao,”.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo kwenye kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na maonesho linalomalizika leo jijini Dar es Salaam.
Amesema kutokana na mabadiliko hayo serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha zinapatikana mbegu za mazao zinazostahili changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo ya ongezeko la joto linalosababisha ukame na baridi.

” Kwa hiyo utafiti unafanyika na tayari ziko aina mbalimbali za mbegu za mazao zinazostahimili ukame na changamoto nyingine zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi na tayari zimezalishwa na zinafikishwa kwa wakulima,” amesema.