Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameahidi kuendeleza kazi na mafanikio yote yaliyofikiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko, ili kuhakikisha azma na maono ya Serikali katika kufanikisha miradi ya kimkakati ifikapo mwaka 2030 yanatimia.
Ndejembi ametoa kauli hiyo leo, Novemba 20, 2025, wakati akipokea rasmi ofisi kutoka kwa Dkt. Biteko katika makao makuu ya Wizara ya Nishati yaliyopo Mtumba, jijini Dodoma.
Ameshukuru kazi kubwa na utendaji uliotukuka wa Dkt. Biteko katika kipindi chote cha uongozi wake.

Amesema kuwa kipindi cha uongozi wa Dkt. Biteko kimeleta mageuzi makubwa katika sekta ya nishati, hususan katika kuboresha huduma, kuongeza ufanisi na kuimarisha tija katika ukuaji wa sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Dkt. Biteko amempongeza Waziri Ndejembi kwa kuteuliwa kuongoza Wizara ya Nishati na kumuahidi ushirikiano wa karibu wakati wowote utakapohitajika ili kufanikisha maono makubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta hiyo.
“Mengi niliyojifunza nikiwa Wizara ya Nishati yamenijenga, lakini kubwa zaidi ni sala zangu kwenu katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku,” amesema Biteko.
Hafla ya makabidhiano hayo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Felchesmi Mramba, pamoja na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati.

