Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Author 17

Viongozi Wa Dini Zote Wajifungie Kuomba,Kujadili Na Kutoa Mapendekezo-SAU

Na Lucy Lyatuu

CHAMA Cha Sauti Ya Umma (SAU)  kimeshauri kuwepo kwa jukwaa litakaloshirikisha   viongozi wa din izote nchini wakijifungia ndani na kufanya  maombi kisha  kujadili  kwa haraka kuhusu hali iliyopo na kutoa mapendekezo  yao kwa wananchi.

Katibu Mkuu wa SAU, Majalio Kyara ambaye  alikuwa  mgombea Urais kupitia chama hicho, amesema hayo Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya uchaguzi  mkuu  uliofanyika Oktoba 29 pamoja na vurugu zilizotokea.

Amesema hiki kipindi sio cha kuongea sana  bali ni wakati wa  kujifungia kutafakari, na ili kujua kipi kifanyike na kwa nini Taifa limefika lilipo lengo likiwa ni kutatua changamoto.

“Wote tunawakubali viongozi wa dini ni rahisi wao wakieleza jambo kueleweka, hivyo wakikaa wakijadili na kujua wapi kuna makosa  itasaidia waliokosa kuomba radhi  na kusamehewa,” amesema na kuongeza kuwa na hata vitabu vya dini vinaeleza ubaya usilipwe kwa ubaya  bali wakiomba radhi wasamehewe.

Amesema ni vyema viongozi hao wakijadiliana kwa haraka sana kabla ya Novemba 25, 2025  ili isifikie huko wanakoeleza 9 Desemba.

“Na hii ningependa tuwatumie zaidi viongozi wa dini, tunaamini hivyo kila mtanzania asilimia 99 ni muislamu au mkristo ambapo viongozi hao wametubeba sisi kwa asilimia kubwa, tukitumia vyama kuna wengine hawana vyama hivyo, tutafute jukwaa la viongozi wetu wa dini zote wote wajifungie ndani, waelezwe na wananchi ambao nao wameshakutana nao wakijua nini kilichotokea na vyombo vya ulinzi vinaweza kuwaeleza  yaliyotokea,” amesema.

 

Amesema hekima na busara za viongozi hao kwa kuwa watakuwa ndani wanaelezwa  watapata picha kama kuna watanzania walitaka kuwa       wasaliti  wataelezwa na kwa pamoja wote watatoka  kwa wananchi kwa msimamo mmoja.

Kyara amesema ni lazima kumtanguliza Mungu mbele akionesha njia, ya namna ya kutoka mahali Taifa lilikofikia  kwa maana hata Rais Samia Suluhu Hassan  alisema fujo zilizotokea zimetia doa.

 

 

 

 

 

 

 

 

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.