Na Lucy Ngowi
DODOMA: HATIMAYE Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imeipokea ndege ya kisasa aina ya Thrush 510P2+ itakayotumika kudhibiti Visumbufu vya mazao, ambavyo ni magonjwa na wadudu waharibifu.
Visumbufu ambavyo vinaathiri uzalishaji wa mazao ya wakulima.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo wakati wa hafla ya mapokezi ya ndege hiyo ambayo baada ya kutua uwanja wa ndege ilipokelewa kwa kumwagiwa maji na magari ya zima moto.
Profesa Ndunguru amesema ujio wa ndege hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wakulima wa Tanzania katika maeneo ya Mbarali, Kapunga, Igunga, Singida, Magu, Simiyu, Manyara, Kondoa, Mvomero, Kilosa na mengineyo, kwa kuwa inawahakikishia mavuno na usalama wa mazao yao.

“Ndege hii imekusudiwa kuongeza ufanisi na wigo katika uchunguzi na udhibiti wa Visumbufu vya mimea nchini.
“Ndege hii imekuja wakati mwafaka wakati Tanzania inahimiza kilimo cha umwagiliaji kinachoenda kufungua mashamba mapya na mengi ya mpunga ambayo moja ya changamoto yake kubwa ni uvamizi wa ndege aina ya kwelea kwelea,” amesema.
Amesema visumbufu vya mimea hususani ndege waharibifu aina ya Kwelea kwelea, nzige na viwavi jeshi vamizi huchangia kwa kiasi kikubwa katika upotevu wa chakula mashambani hivyo kuhatarisha usalama wa chakula nchini na kupunguza tija katika uzalishaji wa mazao.

Amesema ndege hiyo itakuwa nyezo muhimu katika udhibiti wa majanga ya nzige ambayo huikumba Tanzania mara kwa mara na kuhatarisha usalama wa chakula na malisho ya mifugo.
Tanzania imekuwa ikivamiwa na nzige wa aina tatu, nzige Wekundu, Jangwani na Miti. Ndani ya Tanzania kuna maeneo makuu matano ambayo ni mazalia ya Nzige Wekundu yenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 8000. sawa na ekari 1,976,843.
Pia amesema, ndege hiyo pia inaweza kutumia kuzima moto kwenye maeneo makubwa pale unapotokea.
“Ndege hii ina utendakazi wa hali ya juu na imeundwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kilimo ikiwa ni pamoja na kunyunyizia Viuatilifu na mbolea shambani kwa njia ya anga. Pamoja na sifa nyingine ndege hii
Ina tenki la mafuta lenye ujazo wa lita 863 hali inayopelekea ndege kuweza kukaa angani takribani saa manne.

“Ina tenki la Viuatilifu lenye ujazo wa lita 1,930. Kwa uwezo huu, ndege hii inaweza kudhibiti ndege waharibifu wa Kwelea kwelea, viwavijeshi na nzige kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 2400 kwa mara moja.
“Ina vifaa vya kisasa vya redio “Avionics” vinavyoipa uwezo wa kutumika kufanya uchunguzi wa maeneo yenye viashiria vya uwepo wa Visumbufu na taarifa hizo kuaminika na kuwekwa kwenye Mpango wa Unyunyiziaji wa kudhibiti wa Visumbufu katika eneo husika,” amesema.

Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, kwa jitihada za dhati za kutaka kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo yenye malengo ya kuongeza tija, ajira, kupanua na kuimarisha masoko, kuimarisha hali ya chakula na kuimarisha ushirika.
Naye Mwenyekiti Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mariam Ditopile amesema,” Lilipokujq suala la ununuzi wa ndege, tuliona ni maneno maneno.
” Kwa Bunge hili kati ya Wizara ambayo imepokea maoni ya wachangiaji wengi ni Kilimo,” amesema.
Amekiri kwamba suala la wadudu waharibifu hususan Kwelea kwelea lilikuwa linawaumiza wakulima, lakini sasa mkombozi amepatikana.