Na Lucy Ngowi
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amesisitiza kuwa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) linapaswa kujipanga upya, kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, kuwa na uwajibikaji, na kuhakikisha kila mfanyakazi anachangia kwa ufanisi kulingana na nafasi yake.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya kikazi katika ofisi za SIDO mkoani Dar es Salaam, akibainisha umuhimu wa shirika katika kukuza maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati nchini.
Katambi amewapongeza wafanyakazi wa SIDO na kuwaomba wawe wabunifu katika kutambua fursa mpya za kibiashara, kutumia tafiti za awali na mpya kubaini changamoto, na kuhakikisha ushirikiano kati ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati ni nguzo muhimu katika utoaji wa ajira, ukuaji wa uchumi, na kuhakikisha mitaji ya viwanda inabaki ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji, amesema shirika linaendelea kuratibu na kusimamia maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati.
Ameeleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita kuwa ni pamoja na uzalishaji wa mashine na vipuri, kuanzishwa kwa viwanda vipya zaidi ya 2,500, na ongezeko la ajira.
Aidha, SIDO imeendeleza programu ya atamizi wa mawazo bunifu, ambapo mawazo 32 yameatamiwa, pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali, biashara na uchakataji wa bidhaa kwa wajasiriamali.

