Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI Mkuu Mwigulu Nchemba, ametoa onyo kali kwa watumishi wa umma wazembe, wavivu, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa wananchi, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia tabia hizo na ipo tayari kuchukua hatua kali dhidi yao.
Mwigulu ameyasema hayo leo Alhamisi, Novemba 13, 2015 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akitoa shukurani baada ya kuthibitishwa na Bunge kufuatia uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuwa Waziri Mkuu.
“Nawaambia watumishi wote wa umma wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha chafu kwa wananchi tuwe tayari. Nitakuja na fyekeo na rato,” amesema Waziri Mkuu Mwigulu mara baada ya jina lake kuthibitishwa rasmi na Bunge kuwa Waziri Mkuu.

Amesema serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha watanzania wote, hasa wale wa kipato cha chini, wanasikilizwa na kuhudumiwa kwa nidhamu katika kila ofisi ya umma.
“Niwahakikishie Watanzania kila aliye Mtanzania, nchi hii ni yake. Watumishi wa umma watalazimika kwenda kwa wananchi kutatua kero zao badala ya wananchi kufuata ofisini,” amesema.
Pia Mwigulu amesema serikali itashirikiana kwa karibu na wananchi kupitia mapendekezo na hoja mbalimbali, akibainisha kuwa kila sauti, hata ya wachache, itasikilizwa kwa usawa kwa sababu Bunge lililopo ni bunge makini lenye dhamira ya kweli ya kuhudumia Watanzania wote..
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu huyo amewashukuru wabunge kwa kuthibitisha jina lake kushika nafasi hiyo, pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpendekeza, akiahidi kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na juhudi kubwa.
“Majukumu haya si mepesi. Lakini naamini tutayatekeleza yote kama tutamtanguliza Mungu na kuilinda amani ya taifa letu,” amesema.

